Monday, April 21, 2014

ASKOFU AMTAKA LUKUVI ATUBU.

By Jimmy  |  9:49 AM No comments


ASKOFU wa Kanisa la Methodist Jimbo la Dodoma, Joseph Bundala, amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, atubu makosa yake ili asamehewe.
Lukuvi akiwa katika sherehe za kumsimika Askofu Bundala, aliwataka waumini waukatae mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu ya katiba inayojadiliwa na wajumbe wa Bunge Maalumu.
Alisema kama wananchi wakikubali serikali tatu jeshi litashika madaraka na Zanzibar itaukaribisha utawala wa Kiislamu na Waarabu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Askofu Bundala alisema kiongozi imara ni yule anayetubu makosa yake, ili taifa liendelee kuwa na umoja, amani, ushirikiano na utulivu.
Alibainisha kuwa kwa bahati mbaya dunia imejawa na viongozi wasioweza kutubu makosa wala kujiuzulu nyadhifa zao wanapofanya mambo yanayozusha mtafaruku ndani ya jamii.
Alisema wakati Lukuvi akitoa kauli ile, yeye (askofu), alijua italeta mtafaruku mkubwa ndani ya jamii kwakuwa serikali mbili au tatu ni jambo lililo kwenye mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge.
“Kujua kosa ni elimu, viongozi wengi hawana elimu hii, na sisi viongozi wa dini kazi yetu kubwa ni kupigania jambo hili lielewekwe kwa jamii,” alisema.
Alisema viongozi wanapaswa kuchunga ndimi zao, ili matamshi wanayoyatoa yasisababishe mgawanyiko ndani ya jamii.
“Nawaomba Watanzania wamsamehe Lukuvi, mimi sikutarajia angezungumza kauli ile ambayo imezidisha mpasuko ndani ya jamii, nilijua atazungumza mambo ambayo yangewaunganisha zaidi wananchi.
“Najisikia vibaya kuona kauli iliyotolewa na kiongozi tuliyemualika katika kanisa letu imesababisha mvurugano ndani ya jamii, nafikiri ni jambo jema kwa Lukuvi kuomba radhi,” alisema.
Wanasiasa kutumia makanisa
Askofu Bundala, alisema hakuna ubaya kwa viongozi wa siasa kuhudhuria shughuli mbalimbali za kidini, lakini jambo kubwa wanalopaswa kufanya ni kuchunga kauli zao, ili zisije zikazusha mitafaruku.
“Hatuwezi kuacha kuwaalika kwenye shughuli zetu, lakini wanapaswa kujikita katika maudhui yanayofanana na eneo walilopo, masuala ya siasa wakafanye katika majukwaa yao,” alisema.
Mwenendo wa Bunge
Askofu Bundala, alisema haamini kwamba kauli iliyotolewa na Lukuvi kanisani kwao ndiyo iliyochangia wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema tangu mwanzo vikao vya Bunge Maalumu vilionekana kutawaliwa na mabishano, itikadi za kisiasa na misimamo iliyosababisha misuguano mikubwa.
“Sote ni mashahidi Bunge Maalumu halikuwa pamoja tangu wanaanza vikao vyao, kilichotokea pale kanisani kwetu kilikuwa ni hitimisho tu, kama wangekuwa wanaendelea vizuri nina hakika wangemkemea Lukuvi.
“Hawapo pamoja ndiyo maana hata lilipotokea lile la Lukuvi wakaona ndiyo mlango wa kutokea, ninaamini UKAWA watarejea bungeni baada ya kuzungumza na wenzao, hapa ni lazima wafanye maridhiano kuilinda nchi,” alisema.
Awakaribisha UKAWA
Askofu Bundala, alisema anawaunga mkono UKAWA kuamua kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya mchakato wa katiba, lakini waifanye kazi hiyo kwa kutanguliza ukweli na si kuwarubuni wananchi.
“Kama nia ni kutoa elimu tu, hilo ni jambo la kheri kwa kuwa ni lazima wananchi wapate elimu, ili wakifikia hatua ya kupiga kura ya maoni wajue kipi sahihi, UKAWA wakija kuturubuni sitakubaliana nao hata kidogo,” alisema.




Author: Jimmy

Hello, I am Author, decode to know more: In commodo magna nisl, ac porta turpis blandit quis. Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. In commodo magna nisl, ac porta turpis blandit quis. Lorem ipsum dolor sit amet.

0 comments:

E-mail Newsletter

Sign up now to receive breaking news and to hear what's new with us.

Recent Articles

© 2014 Uncle Jimmy | Distributed By My Blogger Themes | Created By BloggerTheme9
TOP