Naomba uambatane na mimi katika kutanua wigo wa
uelewa kwa kuyasoma maisha ya watu wengine katika neno la Mungu kisha Tujifunze
jambo kwa pamoja.
Yeremia 1:6
“Kabla
sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;
nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”
Waamuzi 13:5
“kwani
tazama, Utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume; na wembe usipite juu ya
kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye
ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.”
Katika andiko la awali utagundua ya kwamba Mungu
anazungumza na Yeremia akiwa tayari anaishi, amekwisha kuzaliwa tayari,
na
anamweleza kabla ya kutungwa mimba Yeremia alikuwa anajulikana kwa Mungu
tayari. Ndiyo kusema japo Mungu hakuwaeleza wazazi wa Yeremia au kujifunua kwa
mtu yeyote kueleza kuhusu Yeremia hiyo haiubadalishi mstari wa sita wa sura ya
kwanza kwamba Yeremia alijulikana na Mungu. Kama Mungu alimjua Yeremia uwe na
uhakika alimjua jinsi na kusudi la kuwepo kwake duniani… Kwahiyo wakati mimba
inatungwa, Mungu hakuwa anaona mimba, bali alikuwa anaona nabii wa mataifa.
Kabla wazazi wa Yeremia hawajakutana, Mungu bado alikuwa anaona nabii wa
mataifa. Si kwamba Mungu alianza kumjua Yeremia
baada ya wazazi wake kukutana, bali Mungu aliwakutanisha wazazi wake Yeremia
ili wapate fursa ya kumfahamu Yeremia.
Kwenye andiko linalofuatia ni ujumbe wa malaika
kwa familia ya wanandoa ambao bado walikuwa hawajawahi kupata mtoto maishani
mwao. Malaika anamtokea mama mtarajiwa, ambaye wakati huo alikuwa ni mwanamke
tasa, na anaanza kumpa habari za mtoto wake wa kiume na anaenda hatua ya mbele
zaidi kwa kumweleza kusudi la kuja kwa mwanaume huyo ulimwenguni na namna gani
anapaswa kulelewa… Hii inaweza kuonekana ni habari ya kiuendawazimu kidogo,
kutoa habari kamili juu ya mtoto fulani kwa mwanamke tasa!!! Malaika anatoa
wapi ujasiri wa namna hiyo? Amepewa hizo taarifa na Mungu, kwahiyo malaika
hakuwa anabahatisha au anajaribu kutoa utabiri bali alikuwa anazungumza ukweli,
yaani ndivyo ilivyo. Huyu mtoto wa kiume alikuwa anajulikana kwa Mungu kwahiyo
ilikuwa ni habari sahihi kutoka chanzo sahihi cha habari.
Kwa mwanga wa uelewa huo nilioweka msingi ndani
yako naomba ujiulize je, unadhani kuzaliwa kwako duniani kumemshitukiza Mungu?
Je, Mungu ameshangazwa na uwepo wako (Is God caught by surprise by your
existence?) yaani namaanisha unadhani Mungu amesema “Oooh!!! Kumbe huyu
aliyezaliwa ni James?” au “Ahaa!!! Kumbe leo amezaliwa Sowane?” siku ambapo mimi
nilizaliwa au siku ambapo ndugu Sowane alizaliwa?. Hapana, Yahwe si Mungu mdogo
kiasi hicho eti kwamba kuna matukio yanamshangaza au kumshitukiza! Angekuwa
hivyo, basi asingeweza kuuongoza ulimwengu. Katika lugha ya elimu ya theolojia,
Mungu hutambulishwa kama “omniscient” yaani mwenye ufahamu yote- anayejua mambo
yote!
Natambulisha ufahamu huu ya kwamba kabla ya
kuwepo ulikuwepo na ulijulikana kwa Mungu! Ulikuwa ndani ya mawazo na fikra za
Mungu kabla hujatokea duniani. Ulifahamika jinsi na kusudi la kuwepo kwako
kabla hujadhihirika katika ulimwengu wa mwili. Lakini ni muhimu sana ukarejea
mistari hiyo juu na kuona ya kwamba aliyekuwa ni chanzo cha taarifa za
kuzaliwa, kuishi, kusudi la wanadamu hao alikuwa ni Mungu na hakuna mwingine-
hata malaika! Hiyo ni udhihirisho ya kwamba aliyefanya maamuzi ya jinsi,
nyakati na kusudi la kuzaliwa ni Mungu pekee. Ni dhahiri ya kwamba ukiambiwa
ufikiri ulikuwaje kabla ya kuzaliwa, picha itakayo kuijia mawazoni mwako ni
giza tu! Hukuwa na ufahamu na uelewa na hukuwa na maamuzi ya kuzaliwa kwako.
Binafsi, sikuamua kuzaliwa mtanzania, lakini ile kujua kwamba nimezaliwa kuwa
mtanzania ni furaha sana ndani ya moyo wangu kwasababu ni udhihirisho kwamba
aliyeniweka amekusudia kitu kwa nchi ya Tanzania kupitia mimi na ndiyo maana
akaniweka. Ile kwamba mimi ni mwanaume ninatambua si kwa bahati nzuri au mbaya
bali ni kwa kusudi… Nilijulikana kwa Mungu lakini sikuwa na uwezo na nafasi ya
kufanya maamuzi yoyote na hivyo siwajibiki na maamuzi ya kuzaliwa na kuwepo
kwangu. Hakuna mtu anaweza kunihoji kwanini nilizaliwa mtanzania na si mtu wa
taifa jingine, sipaswi kupongezwa au kulaumiwa kwa kuzaliwa mwanaume, wala
siwajibiki kwa kuzaliwa na kuishi kwangu katika zama hizi. Kwani kuna mtoto
unaweza kumpa hongera au kinyume chake kwa kuzaliwa kipindi cha siasa za vyama
vingi hapa Tanzania? Unadhani kuna mzee wetu yeyote anayestahili kuadhibiwa kwa
kuzaliwa kipindi cha mapambano ya uhuru? Hapana!!! Kwasababu hakuna kati yetu
aliyeshiriki kufanya maamuzi hayo lakini hiyo haiubadili ukweli kwamba sote
tulijulikana kwa Mungu kabla ya kuzaliwa kwetu.
0 comments: