Ongoza kimkakati
Wafilipi 3:12
"Si kwamba
nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili
nipate kulishika lile ambalo kwaajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu."
2Timotheo 4:6
"Kwa
maana,mimi sasa namiminwa,na wakati wa kufariki kwangu umefika.Nimevipiga vita
vilivyo vizuri,mwendo nimeumaliza,
Imani nimeilinda;baada ya hayo nimewekewa
taji ya haki,ambayo Bwana mhukumu wa haki,atanipa siku ile;wala si mimi tu,bali
na watu wote waliopenda kufunuliwa kwake."
Huwezi kusema
umefika au la iwapo hujui unakwenda wapi, vilevile huwezi kukaza mwendo
kuelekea kule usikokujua. “Kuna
umuhimu gani wa kupiga mbio, iwapo hauko katika njia sahihi?"
Kuna kitu
kinachomfanya Mtume Paulo awaandikie Wafilipi kwamba bado hajafika na anakaza
mwendo na anamwandikia Timotheo, mwanae katika imani tuliyonayo kwamba mwendo
ameumaliza kwa tafsiri nyingine ni kwamba hakazi tena mwendo; na kitu hicho ni
malengo.
Je, wajua???.... Malengo hukamilishwa kwa mikakati.
Sifa
kubwa ya malengo ni kuzaa msukumo ndani mwa yule ayabebae wa kuyatekeleza. Kama
malengo hayakusukumi kuanza utendaji, bado hayajawa malengo. Hii ni kwasababu
malengo hayajikamilishi menyewe bali hukamilishwa kwa mikakati.
Mkakati
ni mbinu, hatua madhubuti, wajibu, jukumu… ni utendaji/utembeaji kuelekea
kwenye malengo husika. Kwa ujumla wake, mkakati ni mchanganuo wa
wajibu/majukumu, wahusika, muda wa utekelezaji na rasilimali zinazohitajika
kwaajili ya kukamilisha lengo fulani.
Luka
14:18
"Maana ni nani katika
ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba
anavyo vya kuumaliza?"
Bwana
Yesu anatutambulisha kwenye wazo moja la msingi sana ambalo tunapaswa kujifunza
kwalo kwa moyo na nguvu zetu zote. Anazungumza kwa lugha ya kawaida sana kwa
kutumia mfano wa Ujenzi… Hakuna mtu anayeanza shughuli ya Ujenzi bila kukaa
chini na kuhesabu gharama na kuona kama anavyo vya kuumaliza! Yesu anaposema
“kuhesabu gharama.” Anamaanisha si tu fedha kama ambavyo wengi hudhani moja kwa
moja… Unaweza kuwa na fedha lakini huna muda, watu, nguvu kazi, nafasi n.k
kwahiyo lazima tuelekeze akili zetu kumuelewa Yesu kwa kina na mapana.
Je, unavyo vya kutosha kukamilisha malengo yako?
Jibu la swali huli huzaliwa kwa jinsi ambavyo utatumia muda kufanya uchambuzi
na kutengeneza mkakati.
Kuna watu wengi sana nimewashuhudia na marafiki
zangu kadhaa wamenaswa kwenye mkwamo ambao hata mimi hapo awali nilijikuta
nimekwama na hata sasa ninajuhudi za kupigana vita kepuka mkwamo huo… kuanza
jambo na kutolikamilisha! Mkakati unakusaidia kujinasua kutoka kwenye
mkwamo huo. Ninaomba uambatane nami kuchanganua mambo muhimu ndani ya mkakati.
i.
Wajibu/Jukumu – Huu ni
mchanganuo wa kazi ndogo ndogo ili kulielekea lengo husika.
ii.
Wahusika – Ndani ya mkakati unapaswa
kuainisha nani atahusika kufanya nini. Ni muhimu sana mkakati ufikie hatua ya
kugawa majukumu na wajibu kwa muhusika fulani kwaajili ya utendaji. Kutokana na
aina ya malengo, vyaweza kuwepo vigezo vya kumbebesha mtu fulani wajibu au
jukumu: mfano upatikanaji wake, kipaji, uwezo, uzoefu, ujuzi n.k
iii.
Muda/Wakati – Hii ni
rasilimali muhimu amabayo kila mtu amepewa sawasawa. Kila mtu ana masaa
ishirini na nne (24) ndani ya siku moja,
siku saba ndani ya wiki moja. Kinachojenga tofauti miongoni mwetu ni namna
tunatumia muda wetu. Ni LAZIMA ufanye maamuzi ni muda kiasi gani utahitajika
kwaajili ya kuleta utimilifu wa jukumu fulani. Usidhani utafanya jambo moja
muda wote! Kwahiyo, ni lazima kwa mfano kusema “Nitaandaa rasimu ya
mafundisho/kitabu ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi wa pili yaani tarehe 1- 7
Februari.” Au unaweza kutumia Mchanganuo wa jedwali kama nilivyofundisha hapo
awali na nitaweka mfano huo tena baada ya Maelezo haya juu ya mkakati.
Usipochanganua muda hiyo ni dalili ya kuanza kutumia vibaya muda wako, utaanza
kufanya chochote wakati wowote… jukumu la tisa utaanza nalo, utajikuta
unatamani kufanya jukumu la nne, mara unaona jukumu la saba linaibuka
likifuatiwa na jukumu la kwanza… Hutakuwa na mtiririko maalum! Kwahiyo
utajikuta katika ya mwaka hujafanya chochote cha maana zaidi ya kurukaruka tu
huku na kule.
iv.
Rasilimali fedha –Masikioni
mwa watu wengi sana ukisema rasilimali, huja Taswira ya fedha. Lakini kwangu
binafsi hii huja kama rasilimali ya mwisho… Kwa mfano, unadhani unahitaji fedha
kiasi gani kuandika kitabu??? Hauhitaji hata senti moja kuandika kitabu ila
kuchapisha kitabu ndiyo unahitaji pesa… Sasa,
ni hekima sana kujua ya kwamba kabla ya kitabu kuchapishwa, kwanza
huandikwa! Kwahiyo, usisingizie fedha… Kaa chini uandike. Anza kufanya yaliyo
ndani ya uwezo wako kwanza. Mkakati mzuri ni ule ambao hukusukuma kufanya Mchanganuo
wa rasilimali fedha. Hii hupelekea kujua ni fedha kiasi gani zitahitajika ili
kukamilisha jukumu fulani. Lakini zaidi ya hapo ni lazima kujua kiasi hicho cha
fedha kitahitajika kwa wakati gani. Vilevile, ni muhimu kuainisha vyanzo vyako
vya mapato (jinsi gani fedha hiyo itapatikana) – mshahara, faida ya biashara,
gawio, mkopo, changizo (harambee), ufadhili n.k hii itakusaidia sana kutembea
kwa Uhakika na kutoshangazwa na mambo mengi (not to be caught by surprise).
v.
Nguvu kazi – huu ni uwezo
ulifichika ndani ya mtu (hazina). Uwezo huu huyaleta mawazo katika uhalisia…
Husababisha vitu kuwa halisi. Ni mjumuisho wa ujuzi, Uzoefu, ufahamu na nguvu.
Kwa mfano, ili uwe na kitabu au mafundisho kama haya ni lazima uandishi,
mitindo ya uandishi na utumuzi wa lugha viingie kazini. Lazima kalamu na
karatasi au ipad, kompyuta mpakato n.k vitumiwe na mtu ili kuzalisha matokeo.
Ile Akili, fikra na mawazo ndiyo nguvu kazi. Lazima mkakati wako ukusukume
kutambua na kuyachambua haya kinagaubaga.
Kumbuka,
unafanya uchambuzi wote huo kwa lengo kuu la kujibu swali Je, unavyo vya
kutosha kukamilisha ujenzi wa mnara?
0 comments: